Makala
KUMBUKUMBU YA OGM MIAKA MITANO ILIYOPITA, BARIADI ~SIMIYU NA MATENDO MAKUU YA MUNGU
Ni Miaka mitano imepita sasa, lakini kumbukumbu za Simiyu bado ni hai na halisi kwetu.
Mwaka 2021, tulipokuwa bado wanachuo na wanachama wa CASFETA, tulipata neema ya Kuandaa na kushiriki katika Mkutano Mkubwa wa Injili uliofanyika Wilaya ya Bariadi, Mkoa wa Simiyu, katika vijiji vya Ngulyati na Mbiti, kuanzia tarehe 30 Agosti hadi 5 Septemba 2021.
Haikuwa safari ya kawaida wala hayakuwa matembezi bali Ilikuwa ni safari ya utume & Uinjilisti, upendo na utii kwa agizo kuu la Yesu Kristo la kuhubiri Injili.
Kwa siku saba, tulihubiri Injili, tuliombea wagonjwa na kuwafikia watu waliokuwa na kiu ya kumjua Mungu.
Kwa neema ya Mungu, watu 1,158 walimpokea Yesu Kristo kuwa ni Bwana na Mwokozi wa maisha yao. Wengi walishuhudia nguvu za Mungu kupitia uponyaji, kufunguliwa kutoka katika vifungo mbalimbali na kurejeshewa tumaini.
Leo, baada ya miaka mitano, tunapotazama picha hii ya pamoja, hatuoni sura zetu pekee. Tunaona ushuhuda wa uaminifu wa Mungu. Tunaona maisha yaliyobadilishwa, mioyo iliyoguswa na mbegu za Injili zilizopandwa katika ardhi ya Simiyu.
Tunamshukuru Mungu kwa kila aliyeshiriki, kwa kila aliyeomba, kwa kila aliyetoa, na kwa kila aliyesimama kuhakikisha Injili inawafikia waliokuwa hawajamjua Kristo.
Picha hii si kumbukumbu ya watu waliokutana tu; ni kumbukumbu ya kizazi cha wasomi na wataalamu kilichoamua kuueneza Ufalme wa Mungu kwa Injili na kuacha alama isiyofutika katika maisha ya wengi.
"Basi enendeni mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi..." — Mathayo 28:19
Miaka mitano imepita, lakini utukufu wote unabaki kuwa wa Mungu. Tunamshukuru kwa yale aliyotenda jana, tunamwamini kwa yale anayotenda leo, na tuna matumaini kwa makuu atakayoyafanya kesho.